19 Aprili 2025 - 20:44
Source: Parstoday
Wasiwasi wa Ulaya uliotokana na mgeuko mkubwa katika sera za Marekani kuhusiana na washirika wake

Kubadilika sera za nje za Marekani kumeanza kidogo kidogo kuwatoa mafichoni wanasiasa wa Ulaya kwa kuwafanya waeleze kinagaubaga na kwa uwazi zaidi wasiwasi walionao kuhusu sera za Donald Trump za kujichukulia hatua za upande mmoja.

François Bayrou, Waziri Mkuu wa Ufaransa na mwanasiasa mkongwe wa kihafidhina, ameituhumu Marekani kwa alichokiita "kuutelekeza ulimwengu wa kidemokrasia". Bayrou amesema: "Marekani, ambayo huko nyuma ilijulikana kama mhimili mkuu wa umoja wa mataifa huru na mdhamini wa sheria za kimataifa, imeziweka kando tunu kuu za Magharibi."

Waziri mkuu wa Ufaransa ameuelezea msimamo wa Marekani wa kukaribiana na Russia kuwa ni hatua ya "kushtusha" na akasema, mashinikizo ya Washington kwa Ukraine ya kuitaka isalimu amri haraka kwa matakwa ya Moscow na kutishia kuikatia misaada ya kijeshi Kiev, ni ushahidi wa wazi wa kuwepo mabadiliko makubwa katika sera za Marekani.

Bayrou ameashiria mwenendo wa kutatanisha wa Trump anapoamiliana na Volodymyr Zelensky na malumbano makali ya maneno yaliyozuka baina yake na rais huyo wa Ukraine wakati walipokutana mwezi Februari katika Ikulu ya White House, na akasema: "dunia imeshuhudia kusambaratika kwa miungano, kwa kiwango ambacho hakuna yeyote ambaye angeweza kufikiria."

Wasiwasi wa Ulaya uliotokana na mgeuko mkubwa katika sera za Marekani kuhusiana na washirika wake

Matamshi ya waziri mkuu wa Ufaransa kuhusu kukaribiana zaidi Marekani na Russia na "kutelekezwa na Washington ulimwengu wa kidemokrasia" yanaakisi wasiwasi unaozidi kuongezeka barani Ulaya kuhusu mabadiliko yanayojiri katika sera za nje za Marekani chini ya utawala wa Trump. Mabadiliko hayo yameitia doa kubwa hali ya kuaminiana iliyoko katika uhusiano wa pande hizo mbili za Atlantiki.

Kwa miongo kadhaa, Marekani ilikuwa imejionyesha kuwa ni mtetezi wa tunu za kiliberali, haki za binadamu, na mamlaka ya kujitawala ya mataifa; lakini hivi sasa sera mpya za Ikulu ya White House zimezipa kisogo tunu hizo na kujielekeza kwenye milingano ya kijiopolitiki na kujali zaidi masuala ya kimanufaa na kimaslahi. Zinavyoamini nchi za Ulaya, kuishinikiza Ukraine isalimu amri na kutishia kuikatia misaada ya kijeshi kunakinzana na historia yao ya tangu na tangu ya kuunga mkono serikali za kidemokrasia katika kukabiliana na uvamizi wa kigeni.

Ukraine ni moja ya nchi ambazo zimeathirika zaidi na mgeuko huo wa sera za Marekani. Kwa mujibu wa Taasisi ya Taaluma za Ukraine katika Chuo Kikuu cha Harvard, kitisho cha kukatwa misaada ya kijeshi ya Marekani na kuishinikiza Ukraine ikubali matakwa ya Russia kumeiweka nchi hiyo katika hali ngumu. Jambo hilo sio tu limehatarisha usalama wa taifa wa Ukraine, lakini pia limeifanya nchi hiyo iamue kutafuta msaada na uungaji mkono mpya kwa za nchi za Ulaya.

Baadhi ya wachambuzi wa barani Ulaya wanaamini kuwa kuna uwezekano wa serikali Trump kufikia makubaliano na Russia ambayo yataifanya Ukraine ilazimike kusamehe sehemu ya ardhi yake na kutupiliwa mbali pia suala la nchi hiyo kujiunga na NATO.  Kwa mtazamo wa Ulaya, makubaliano kama hayo, sio tu ni sawa na kuisaliti Ukraine, lakini pia yanakiuka misingi ya mamlaka ya kujitawala kitaifa na umoja wa ardhi yote ya nchi hiyo.

Wasiwasi wa Ulaya uliotokana na mgeuko mkubwa katika sera za Marekani kuhusiana na washirika wake

Japokuwa wasiwasi ulioonyeshwa na Bayrou ni dukuduku la pamoja la nchi nyingi za Ulaya, lakini tusighafilike na mgawanyiko uliojitokeza pia ndani ya Umoja wa Ulaya. Baadhi ya nchi, hasa katika Ulaya ya Mashariki, zina wasiwasi mkubwa zaidi kuhusiana na tishio la Russia na zina msimamo mkali zaidi dhidi ya nchi hiyo.

Lakini baadhi ya nyingine, zinapendelea zaidi kuwa na maelewano na Moscow kwa sababu za kiuchumi au za kisiasa.

Tofauti hizo zinaweza kuwa kizuizi kwa Ulaya kufuata muelekeo wa pamoja na kuchukua msimamo mmoja na athirifu katika kuamiliana na Russia na Marekani. Ufaransa, ambayo ni mmoja wa wadau wakuu wa Ulaya ina wasiwasi kwamba ikiwa Marekani itajivua jukumu lake uongozi wa kulinda mfumo wa dunia wa baada ya zama za Vita vya Pili vya Dunia mpasuko wa kijiopolitiki uliojitokeza kati ya Washington na Brussels utapanuka zaidi. Hali hiyo inaufanya Umoja wa Ulaya ulazimike kubuni tafsiri mpya ya sera za kujitegemea za ulinzi na usalama.

Matamshi ya Bayrou yanaonyesha kuwa uhusiano wa Marekani na Ulaya unapita katika kipindi cha mvutano mkubwa na cha hali tatanishi. Wakati viongozi wengi wa Ulaya wana matumaini kwamba mvutano huo utakuwa ni wa muda tu na uhusiano baina ya pande mbili za Atlantiki utarejea katika hali ya kawaida, baadhi yao wana wasiwasi juu ya mabadiliko ya kimuundo yaliyojitokeza katika sera za nje za Marekani na kupungua utekelezwaji wa ahadi ilizotoa Washington kwa mataifa ya Ulaya…/

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha